Utangulizi
Unaweza kuwa na shinikizo la damu (presha) kwa muda mrefu bila kuwa na
dalili zozote. Muda wote huu ingawa unakuwa hauna dalili, uwepo wa shinikizo la
damu huendelea kuathiri mishipa ya damu na kusababisha madhara makubwa mwilini
kama vile magonjwa ya moyo na kiharusi. Hivyo
ni vizuri kujipima mara kwa mara ili kuepuka kuchelewa.
Shinikizo la damu hutokea taratibu kwa kadri umri unavyozidi
kuongezeka, hivyo kuathiri karibu kila mtu anapofikia umri mkubwa. Upimaji wake
ni rahisi kwa hiyo ni vema ukapima ili kuweza kupambana na ugonjwa huu kwa
msaada wa daktari.
Dalili
Watu wengi wana shinikizo la damu bila kujua au kuwa na dalili.
Ni wachahe wanaweza kuwa na dalili kama vile kuumwa kichwa,kutokwa na damu
puani na kupata shida ya kupumua. Dalili hizi si maalumu (spesific) na mara nyingi
hazitokei mpaka shinikizo linapokuwa katika kiwango kinachohatarisha maisha.
Shinikizo la damu hutokea kwa namna mbili;
Kwanza: Hutokea bila uwepo wa ugonjwa sababishi. Hii ni kwa
sababu tu ya mishipa kupoteza uwezo wake wa kutanuka kutokana na umri.
Pili: Hutokea panapokuwa na ugonjwa sababishi kama vile;
·
Ugonjwa wa figo
·
Kansa ya tezi iliyo juu ya figo
·
Magonjwa ya kuzaliwa ya mishipa
·
Unene kupindukia
·
Matumizi ya dawa kama vile dawa za maumivu,dawa
za mafua,dawa za uzazi wa mpango n.k
·
Matumizi ya dawa za kulevya kama vile kokeini na
amfetamini.
Sababu
·
Umri. Wanaume wana uwezekano mkubwa wa kupata
shinikizo la damu mapema zaidi ya wanawake. ( wanaume chini ya miaka 64,
wanawake baada ya miaka 65). Lakini ni vema kujua kuwa unaweza kupata ugonjwa
huu katika umri wowote
·
Historia ya familia. Presha ni miongoni mwa
magonjwa ya kurithi.
· Matumizi ya tumbaku. Kemikali zilizopo kwenye
tumbaku huharibu kuta za mishipa ya damu. Kuta zlizoharibika hazina uwezo wa
kutanuka vizuri hivyo husababisha mtiririko wa damu kuwa mgumu.
·
Chumvi. Madini ya sodiam katika chumvi huvuta
maji ndani ya mishipa ya damu na kusababisha shinikizo.
·
Unene wa kupindukia. Kadiri unavyozidi kuwa mnene
ndivyo mfumo wa damu unavyozidi kuhitaji damu nyingi ili kulisha sehemu zote za
mwili. Damu nyingi husababisha shinikizo.
·
Kuishi kwa kukaa bila mazoezi. Maisha ya kukaa bila kufanya mazoezi au kufanya kazi inayoongeza mapigo ya moyo yanachangia kupata presha.
· Msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo husababisha
kutolewa kwa homoni ya kotizoni inayochangia kupandisha presha na kiwango cha
sukari mwilini.
·
Uwepo wa magonjwa sugu kama
vile figo, kisukari, unene n.k.
Madhara ya Shinikizo la Damu
Shinikizo la damu katika mishipa ya damu husababisha kuharibika kwa viungo mbalimbali vya mwili.
Uharibifu huu huenda sambamba na kadiri presha inavyozidi
kuwa ya juu na isipotibiwa kwa kuda mrefu.
Madhara yake ni kama ifuatavyo;
- Kiharusi au mshtuko wa moyo
- Kupasuka kwa mishipa ya damu
- Mtindio wa ubongo
- Kisukari
- Kupoteza kumbukumbu n.k.
Upimaji wa shinikizo la damu
Vipimo vya shinikizo la damu kitaalamu vimegawanywa katika sehemu nne;
- Kipimo cha kawaida ambacho ni chini au sawa na 120 mm za mekyuri kwa kipimo cha juu na chini au sawa na 80 mm za mekyuri kwa kipimo cha chini, kwa kifupi huandikwa 120/80mmHg
- Kupanda kwa mgandamızo wa damu: 120-129/80 mmHg
- Shinikizo la damu hatua ya kwanza: 130-139/80-89 mmHg
- Shinikizo la damu hatua ya pili: 140 au zaidi/90 au zaidi mmHg
Ikumbukwe kuwa upimaji huu lazima ufanywe mara tatu au zaidi kwa nyakati tofauti ili kupata matokeo sahihi. Wakati mwingine daktari hushauri ufuatiliaji wa kipimo cha shinikizo la damu kwa masaa 24 ili kujua mwenendo na visababishi kwa dhumuni la kuanzisha tiba sahihi ikiwemo kubadilisha jinsi mtu anavyoishi au dawa.
Tiba
Mara nyingi shinikizo la damu katika hatua za mwanzo huanza kutibiwa kwa kubadilisha mwenendo wa maisha ya mgonjwa kama vile;
- Kula chakula chenye mlo kamili na kupunguka matumizi ya chumvi,
- Kufanya mazoezi ili kuimarisha mishipa pamoja na moyo,
- Kupunguza uzito ,
- Kupunguza au kuacha kunywa pombe na kuvuta sigara.
Hizo ni miongoni mwa hatua chache ambazo mgonjwa au hata mtu mwenye afya anaweza kuzichukua ili kuzuia kupata shinikizo la damu pamoja na madhara yake.
Endapo ugonjwa huu utashindikana kudhibitiwa kwa njia hizi basi daktari anaweza kukuanzishia dawa. Lakini kumbuka kinga ni bora kuliko tiba.
Hili moja ya machapisho muhimu sana katika kuelimisha jamii!
JibuFutaChapisho limetoa mwongozo sahihi juu ya maradhi ambayo kwa asilimia kubwa huwakumba jamii yetu. Ni somo zuri sana nimelipenda kiukweli.