Utangulizi
Kichaa cha mbwa ni nini?
Ni ugonjwa hatari unaotokana na maambukizi ya virusi vijulikanavyo kama rabies kwa kiingereza. Maambukizi hayo hutokea baada ya kung'atwa, kukwaruzwa na makucha au kulambwa machoni,puani, mdomoni au katika jeraha na mbwa, paka au popo aliye na virusi hivyo.
Tofauti na virusi,unapong'atwa na mbwa au paka ni hatari ya kupata maambukizi ya bakteria katika majeraha ambayo husababisha maumivu makali na kuchelewesha kupona kwa majeraha hayo kama hatua hazitachukuliwa haraka. Lakini pia kupata majeraha sehemu za viungo(joints) kunaweza kumsababishia mgonjwa ulemavu wa kudumu.
Nchini Tanzania pekee inasadikiwa kuwa watu 1500 hufariki kila mwaka kutokana na kichaa cha mbwa, ugonjwa unaoweza kuzuiwa kwa asilimia 100 kwa kutumia chanjo(DW).
Nini cha kufanya unaposhambuliwa na mbwa, paka au popo?
Kuna hatua muhimu kadhaa za kufanya pindi unaposhambuliwa na mbwa, paka au popo.
- Safisha majeraha kwa maji yanayotiririka na sabuni bila kusugua kwa dakika tano hadi kumi,
- Paka mafuta ya antibayotik kama unayo, epuka kupaka mafuta ya mgando,mafuta ya taa, mkojo au kitu kingine chochote zaidi ya mafuta ya antibayotik,
- Punguza kutokwa na damu kwa majeraha kwa kufunga kwa kipande kisafi cha nguo au bandeji mpaka pale utakapomuona daktari,
- Hakikisha unamuuliza mmiliki kama mbwa huyo ana chanjo na ikiwezekana akuonyeshe kadi ya chanjo, na kama ni mbwa koko au anayejulikana kuwa na ugonjwa basi ni vyema ukawahi haraka iwezekanavyo kwenda kliniki.
Yatakayofanyika hospitalini
Daktari au manesi wauguzi watakusafisha majeraha tena na kukuchoma sindano za chanjo za kichaa cha mbwa na tetenasi. Pia wataangalia kama majeraha hayo yanafaa kushonwa hasa majeraha ya usoni au majeraha makubwa, lakini mara nyingi majeraha hayo kuachwa wazi. Pia kuna uwezekano mkubwa kuwa utaanzishiwa dama za maumivu na antibayotik.
Dalili za kichaa cha mbwa
- mafua ya ghafla,
- homa kali na maumivu ya misuli,
- kupata ganzi sehemu ya jeraha,
- kukosa hamu ya kula,kichefuchefu na kutapika,
- kukosa nguvu au kuparalaizi kwa misuli hasa ya koo, taya, mfumo wa upumuaji na miguu na mikono,
- kuwa na dalili za pindupindu(seizure),
- kuongea vitu visivyojulikana,
- kupata tabu ya kupumua.
Pindi utakapokuwa na dalili hizi daktari atalazimika kukurifaa au kukulaza kwa matibabu zaidi.
Kama hauna dalili hizo hapo juu na haukulazwa hospitali hakikisha unatumia dawa ulizoandikiwa hadi ziishe na kusafisha vidonda mara kwa mara . Rudi tena kwa daktari baada ya kumaliza dawa ili kufanyiwa uchunguzi tena na kujua kama kuna ulazima wa kuendeleza dozi au la.
Namna ya kujikinga na Kichaa cha Mbwa
- Mbwa na paka ni lazima wawe wanafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara na kuchanjwa,
- Ripoti mbwa ambaye anaonyesha dalili zisizo za kawaida kama kuwa mkali na kushambulia watu bila kubughudhiwa na kuwatenga mbwa na paka wote wa eneo hilo,
- Usimsumbue mbwa anapokula au kulisha watoto wake,
- Usimpige mbwa, kumvuta mkia au kumrushia mawe,
- Kimbilia hospitali unapong'atwa na mbwa ili kupata tiba.
Ni vigumu kufahamu kama wanyama hao wana virusi au la kwani sio kila wakati huonyesha dalili za ugonjwa huo. Usipotibiwa kwa wakati ugonjwa huu kushambulia mfumo wa fahamu na kushababisha mtindio wa akili au hata kifo. Kumbuka kinga ni bora kuliko tiba.
Maoni
Chapisha Maoni