Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Msongo wa Mawazo (Depression)


Msongo wa mawazo ni nini?

Msongo wa mawazo  (Depression) ni mfadhaiko wa akili anaoupata mtu kutokana na shida, taabu, dhiki, matatizo au changamoto zinazomkabili katika maisha ya kila siku. Msongo wa mawazo hutokana na pale mtu anaposhindwa kukabiliana na jambo linalomtatiza. Msongo wa mawazo huwapata watu wa rika na asili zote. Tafiti zinaonyesha kuwa wanawake  hupata msongo wa  mawazo zaidi kuliko wanaume. Msongo wa mawazo ni tatizo la kimwili pamoja na kiakili.

Dalili.
  • kujisikia maumivu sehemu mbalimbali za mwili hasa kichwa,
  • kukosa hamu ya kula au kula chakula kupitiliza,hasa vyakula vyenye madhara,
  • kukosa hamu ya tendo la ndoa,
  • kuwa na huzuni wakati wote na kujisikia mnyonge,
  • kusahau kirahisi au kupungua kwa uwezo wa kufikiria,
  • kujisikia mpweke au kukosa matumaini ya maisha,
  • kupungua kwa uwezo wa kimasomo kwa wanafunzi,
  • kuwa na hofu au kutokujiamini,
  • kupungua au kuongezeka uzito bila kupenda,
  • kushindwa kulala au kulala kupindukia,
  • kukosa utulivu wa nafsi,
  • kubadilika kwa siku za hedhi au kutokupata hedhi kabisa,
  • kubadilika kwa mwenendo ghafla k.v kugombana na ndugu, jamaa au marafiki bila sababu za msingi, kunywa pombe kupindukia au kutumia madawa ya kulevya,
  • kuwa na mawazo ya kujidhuru au kujiua.
Ili dalili hizi zihesabike kuwa ni msongo wa mawazo, kitaalamu ni lazima mtu azionyeshe kwa muda wa wiki mbili au zaidi. Kwa mfano, huzuni anayokuwa nayo mtu aliyefiwa huhesabika kama msongo wa mawazo kama itachukua wiki mbili au zaidi. Watoto wadogo wanaweza kuonyesha dalili tofauti na zile zilizotajwa hapo juu. 

Sababu.
Sababu za msongo wa mawazo  zimegawanyika katika makundi mawili ambazo ni kisaikolojia na kibayolojia. 

1.Sababu za kibayolojia.
  • Magonjwa sugu kama vile UKIMWI, figo, moyo, ini, TB, kisukari n.k,
  • Mtu kurithi vinasaba kutoka kwa mzazi/ wazazi.
2.Sababu za kisaikolojia.
  • Matukio yasiyofurahisha kama Ubakaji,Uvamizi, Ajali au Kufiwa, kutekwa nyara, 
  • Majanga kama Kimbunga, Mafuriko, Tetemeko la ardhi n.k,
  • Changamoto za kila siku za maisha kama vile Ugoni, Talaka, Mimba kuharibika, Kutoa mimba, Kutengana, Kufungwa, Kuuguza au Kukosa kazi, Ugomvi kwa wanandoa, Kusingiziwa jambo, Ushirikina n.k,
  • Matatizo sehemu za kazi Kufukuzwa kazi / Chuo, Migogoro kazini au Kustaafu kazi,
  • Mambo ambayo yanategemewa mtu kufurahi yanaweza kumsababishia msongo wa mawazo kama Kuoa au Kuolewa, Kuzaliwa mtoto, Kufaulu mtihani, Ajira mpya, kuhamia nyumba mpya, Kupata ujauzito nk. 

Namna ya kupunguza Msongo wa Mawazo
  • Tafuta chanzo cha msongo na epukana nacho,kabiliana nacho au kubaliana nacho, 
  •  Kuwa na mtazamo chanya kwamba hiyo ni changamoto inayokukabili na sio mwisho wa maisha, 
  •  Fanya mazoezi ili kupunguza mzigo wa hisia unaokuelemea na kuondoa msongo wa mawazo, 
  •  Epuka kuwa peke yako, washirikishe watu wa karibu matatizo yako na kuomba ushauri,
  • Pata muda wa kutosha wa kupumzika ikiwa ni pamoja na kulala, 
  • Epuka mazoea mabaya kama kunywa pombe au kutumia dawa kwa imani kwamba zitakupunguzia msongo wa mawazo, 
  • Jitahidi kula vizuri kwani mwili unategemea chakula ili uweze kufanya kazi vizuri, 
  •  Fanya vitu ambavyo vitakupa starehe kama kusoma vitabu, kusikiliza mziki, kwenda sehemu za burudani, na kuwa na mtu wa kukufariji. 
  •  Badilisha mazingira kwa kutembelea sehemu mbalimbali kama vile fukwe za bahari, mbuga za wanyama, bustani nk, 
  • Pata ushauri wa wataalamu (daktari, mwanasaikolojia nk), 
  •  Kutumia dawa kwa usahihi kila wakati na 
  •  Kuhudhuria kiliniki kila wakati kama ulivyopangiwa na wataalamu wa afya.
Hitimisho.
Msongo wa mawazo ni  ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine na ni janga kubwa ambalo jamii zetu hatulitilii maanani. Watu wengi wamepoteza ndugu na jamaa kwa sababu ya msongo wa mawazo lakini mara nyingi tatizo hili huunganishwa na matukio mengine. Elimu zaidi juu ya msongo wa mawazo inahitajika katika jamii uli kuongeza ufahamu na kukabiliana na ugonjwa huu.

Vyanzo.

Maoni

  1. Asante kwa Elimu keep the good work up

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ualbino (Albinism)

 Ualbino ni nini? Ualbino ( albinism ) ni hali ya kiafya inayotokana na mwili kukosa uwezo wa kutoa homoni aina ya melanin . Homoni hii pamoja na kazi nyingine inahusika na utoaji wa rangi ya mwili. Ukosefu wa melanin huathiri ngozi, macho na nywele.  Ualbino ni hali ya kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ikumbukwe kuwa  Albino sio mgonjwa bali ni mlemavu wa macho, nywele na ngozi ambavyo huathiri maisha yake ya kila siku, hata kufupisha umri wa kuishi. Nje na binadamu ualbino unaathiri pia wanyama, samaki, wadudu, nyoka, mijusi, ndege na hata mimea (kwa mimea hutokana na ukosefu wa klorofili).  Waathiriwa wenyewe nchini Tanzania waliamua kupendelea kuitwa "watu wenye ualbino" kutokana na matumizi mabaya ya neno zeruzeru katika utamaduni wa Afrika ya Mashariki ambako watu mara nyingi waliona uhusiano kati ya waathiriwa na mapepo au mizimu. Kuenea kwa Ualbino Tafiti zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya 20,000 duniani ni albino, lakini kwa sababu zisizofahamika ba...

Ugonjwa wa Fistula ( Rectovaginal Fistula)

  Fistula ni nini? Fistula ni tundu lisilo la kawaida ambalo hutokana na kuungana kwa sehemu ya chini ya utumbo mpana (njia ya haja kubwa) na njia ya mkojo au njia ya uke, hivyo kumfanya mgonjwa kushindwa kuzuia haja au kutokwa na hajak ubwa ukeni.  Mara nyingi husababishwa na kujeruhiwa kwa sehemu hizo wakati wa kujifungua hasa kwa wanawake wanaozaa katika umri mdogo au wanaokosa msaada stahiki wakati wa kuzaa. Kwa mujibu wa shirika la afya duniani,  inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na Asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote, kwa upande wa Tanzania wengi wamekua wakitafuta msaada kwa waganga wa jadi.   Nini Husababisha Fistula? Ugonjwa wa Fistula unaweza kusababishwa na mambo kadhaa ikiwemo yafuatayo; Majeraha wakati wa kujifungua, Maambukizi ya Mfumo wa uzazi (PID), Mgonjwa ya utumbo mpana kama vile Crohn , Saratani ya mfumo wa uzazi au utumbo mpana, Majeraha yanayotokana na ajali au upasuaji wa sehemu ya nyonga. Fi...

Homa ya Mfumo wa Uzazi (Pelvic Inflamatory Disease- PID )

Homa ya Mfuko wa Uzazi ni nini? Ni magonjwa yanayompata mwanamke katika uke, shingo ya uzazi,mfuko wa uzazi, mirija ya uzazi na sehemu inayozunguka mfumo wa uzazi. Karibu asilimia 85 ya watu wanaopata homa hii hutokana na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana, wengi wao wakiwa na vimelea vya bakteria kama vile  kisonono (gonorrhoea) , kaswende (syphilis) , klamidya n.k. Wakati mwingine mgonjwa hupata homa hii kutokana na bakteria ambao kawaida huwa wapo mwilini na hawana madhara lakini kwa sababu mbalimbali kama kupungua kwa kinga, kisukari, saratani, upasuaji, kuwa na magonjwa ya mfumo wa chakula n.k wanasababisha homa.   Dalili Maumivu makali chini ya kitovu na kiunoni, Maumivu wakati wa tendo la ndoa, Maumivu wakati wa kukojoa, Maumivu makali au kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi, Kutokwa na majimaji yenye harufu kali  na rangi ya njano, kijani au kahawia ukeni, Kuwa na homa jotoridi 38.3 au zaidi, Kujisikia uchovu, kichefuchefu n.k.   Sababu Homa ya...