Utangulizi
Unapokula chakula cha wanga kama vile ugali,wali, matoke,mihogo,viazi n.k hubadilishwa kuwa sukari iitwayo glukozi. Glukozi ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya nishati.Sukari hii hudhibitiwa na homoni iitwayo insulini,inayotolewa na kiungo kinachoitwa kongosho kilichopo katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.
Kisukari ni ugonjwa unaosababisha na mwili kushindwa kubadili glukozi kuwa nishati,hivyo kusababisha kiwango cha sukari kuwa kingi katika mzunguko wa damu. Kwa lugha ya kitaalamu huitwa Diabetes Mellitus.Kuna aina nyingi za kisukari lakini kwa kurahisisha,kwa leo tutagawanya katika aina kuu tatu.
Aina ya kwanza
Pia huitwa inslini tegemezi. Kongosho hushambuliwa na magonjwa ya kingamaradhi(autoimmune) na kushindwa kutoa homoni ya insulini. Kisukari cha aina hii humpata mtu akiwa katika umri mdogo. Dawa yake ni mgonjwa kupatiwa insulini.
Aina ya pili
Huu ni ugonjwa wa kurithi. Aina hii huwapata zaidi watu wanene na wanene kupindukia. Watu wanene wana kiasi kikubwa cha matufa mwilini. Mafuta huzuia insulini kubadili sukari kuwa nishati. Aina hii ya kisukari huwapata zaidi watu wazima,ingawa miaka ya hivi karibuni idadi ya vijana wenye aina ya pili ya kisukari wameongezeka duniani kutokana na kuwa wanene, kukosa lishe bora na mazoezi.
Aina ya tatu
Aina hii huwapata wajawazito. Ujauzito husababisha mabadiliko makubwa ya homoni mwilini ikiwa ni pamoja na kuzuia insulini kufanya kazi. Asilimia 2 hadi 10 ya wanawake hupata kisukari cha aina hii wakati wa ujauzito hasa kuanzia wiki ya 24 na kuendelea. Wengi wao hupona baada ya kujifungua, ingawa wachache hupata aina ya pili ya kisukari wiki au hata miaka kadhaa baada ya kujifungua.
Dalili
- Kuongezeka kwa hamu ya kula na kiu kupita kiasi,
- Kupungua uzito ingawa unakula chakula (aina ya kwanza),
- Mdomo kuwa mkavu,
- Kukojoa mara kwa mara,
- Kuchoka kupita kiasi,
- Kupungua uwezo wa kuona,
- Vidonda kutokupona haraka,
- Kukosa hamu ya tendo la ndoa,
- Kupata maradhi ya njia ya mkojo mara kwa mara kwa wanawake.
Wajawazito wengi hawapati dalili zozote wa kisukari. Mgonjwa hujulikana kutokana na vipimo pale anapoenda kliniki kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Vipimo
Pindi unapokuwa na dalili za kisukari,daktari atakupima kwa kutumia damu kama ifuatavyo ;
Aina ya kipimo | Kiasi cha kawaida | Kiwango hatarishi | kisukari |
Wakati una njaa* | Chini ya 100 | 100-125 | 126 na zaidi |
Wakati umeshiba | Chini ya 140 | 140-199 | 200 na zaidi |
Kipimo cha hemoglobini A1c | Chini ya %5.7 | %5.7-6.4 | %6.5 na zaidi |
*Ukiwa hujala chakula kwa masaa 10 hadi 12.
Pindi unapogundulika kuwa una kisukari, daktari atakupa ushauri na kukuanzishia tiba kutokana na aina ya kisukari ulicho nacho.
Vitu vinavyochangia kupata kisukari;
- Unene,
- Umri-kadri umri unavyoongezeka una hatari ya kupata kisukari
- Msongo wa mawazo,
- Shinikizo la damu,
- Asili-watu weusi,wahispania na wahindi wana hatari ya kupata kisukari zaidi ya asili zingine.
Madhara ya kisukari
- Hatari ya kupata magonjwa ya moyo,shinikizo la damu,kiharusi na magonjwa ya mishipa ya damu,
- Kisukari huharibu mishipa ya fahamu na hivyo kumsababishia mgonjwa kupata ganzi,maumivu na kuhisi miguu kuwaka moto.
- Kushambuliwa kwa viungo muhimu kama figo,macho na ubongo. Hivyo kusababisha figo kushindwa kufanya kazi(kidney failure), upofu na mtindio wa ubongo.
- Vidonda kutokupona
- Kupata magonjwa ya ngozi na njia ya mkojo.
Kinga
Ingawa aina ya pili ya kisukari ni ugonjwa wa kurithi,kuna baadhi ya hatua ambazo zikichukuliwa humsaidia mtu kuepuka kupata au kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa huu;
- Epuka kula vyakula vya mafuta kupita kiasi,
- Fanya mazoezi kuzuia kunenepa,
- Epuka msongo wa mawazo,
- Punguza au epuka kunywa pombe,
- Epuka uvutaji wa sigara,
- Lala usingizi wa kutosha.
Tiba
Tiba dhidi ya kisukari hupangiliwa kutokana na aina ya kisukari, kiwango cha sukari na umri wa mgonjwa.
Kwa ufupi aina ya kwanza ya kisukari dawa yake ni inslini na aina ya pili na tatu ya kisukari ni dawa ambazo husaidia insulini kupenya katika tishu na kuongeza nguvu ya insulini kufanya kazi.
Hitimisho
Kisukari ni ugonjwa unaozuilika,cha kufanya ni kuepuka hulka hatarishi na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya. Lakini ikumbukwe kuwa siku zote kinga ni bora kuliko tiba.
Maoni
Chapisha Maoni