Utangulizi
Mshtuko wa Moyo hutokea wakati mshipa au mishipa ya damu inayoenda kwenye misuli ya moyo inapoziba na kushindwa kuipatia oksijeni misuli hiyo. Mishipa hiyo huziba kutokana na kuongezeka kwa mafuta aina ya kolesterol kwenye kuta za mishipa hiyo iitwayo coronary arteries.
Mshtuko wa moyo ni tatizo la dharura ambalo lisiposhughulikiwa kwa haraka husababisha kifo.
Dalili
- Kupata maumivu makali ya kifua, mikono hasa wa kushoto,shingoni, mgongoni au kwenye taya ghafla na kuhisi kama kugandamizwa na kitu kizito kifuani,
- Kuhisi kichefu chefu,maumivu ya tumbo,
- Kutokwa na jasho la baridi,
- Kupatwa na kizunguzungu,
- Kuhisi uchovu wa ghafla,
- Kushindwa kupumua.
Sio kila mtu hupatwa na dalili hizi. Wengine husikia maumivu kidogo huku wengine dalili ya kwanza ni moyo kusimama.Lakini mara nyingi mtu akipatwa na dalili kadhaa kati ya hizo hapo juu kuna uwezekano mkubwa kuwa amepatwa na mshtuko wa moyo.
Sababu
Kama nilivyosema kwenye utangulizi,mshtuko wa moyo hutokea baada ya misuli ya moyo kukosa hewa ya oksijen. Hii hutokea kwa sababu mbalimbali kama vile;
- Mishipa kuziba kutokana na kuwa na mafuta mengi ndani yake,
- Mishipa ya damu kusinyaa,
- Damu kuganda ndani ya mishipa,
- Misuli kuwa mikubwa kutokana na ugonjwa sugu wa moyo(chronic heart failure).
Watu wenye hatari ya kupata mshtuko wa moyo;
- Watu wanene-hutokana na wao kuwa na mafuta mengi katika viungo kama vile maini,moyo,mishipa na ngozi,
- Watu wenye kisukari- kisukari huzuia mwili kutumia mafuta hivyo kusababisha limbikizo la mafuta. Lakini pia sukari nyingi husababisha damu kuwa nzito hivyo kuhatarisha mishipa kuziba,
- Watu wenye shinikizo la damu,
- Uvutaji wa sigara,
- Umri-kadri umri unavyoongezeka ndio kuna hatarishi ya kupata mshtuko wa moyo,
- Matumizi ya madawa ya kulevya kama kokain ,
- Historia ya familia- mshtuko wa moyo ni miongoni mwa magonjwa ya kurithi ingawa sababu zake bado hazijulikani kitaalamu,
- Msongo wa mawazo,
- Kukosa mazoezi.
Nini cha kufanya unapohisi dalili:
Kama mtu aliye karibu yako ana maumivu makubwa ya kifua au dalili hizo hapo juu;
- Piga simu namba 114 (kwa Tanzania) kama hakuna uwezekano wa kuja ambulansi kama vile trafiki kubwa au vijijini mkimbize hospitali au kituo cha afya kilicho karibu na hapo ulipo.
- Kama inawezekana mpe kidonge kimoja cha aspirini (100 hadi 300 mg) atafune.
- Kama mgonjwa anajulikana kuwa na ugonjwa wa moyo na ana dawa zake anaweza kutumia kidonge cha nitroglycerine.
Dawa za maumivu kama ibuprofen au panadol hazina faida na zinaweza kuleta madhara zaidi.
Msaada wa haraka kwa mwenye mshtuko wa moyo unahitajika ili kuokoa moyo pamoja na kuepuka kuharibika kwa misuli au mfumo wa umeme wa moyo.
Kama ilivyo kwa magonjwa mengi sugu unaweza kuepuka mshtuko wa moyo kwa kuzingatia afya yako kama vile;
- Kufanya mazoezi
- Kula chakula bora na mlo kamili
- Kupima mara kwa mara vitu kama kiasi cha mafuta(Kolesterol,Trigliserid), sukari, Pressure na mapigo ya moyo
- Kuepuka vitu hatarishi kama uvutaji wa sigara,matumizi ya madawa ya kuvevya nk
- Kwa wenye magonjwa sugu kama magonjwa ya moyo,kisukari,presha,figo, homa ya ini nk watumie dawa kama walivyoshauriwa na madaktari wao na pindi wanapohisi dalili mbalimbali waende kituo cha afya kilicho karibu nao.
Maoni
Chapisha Maoni