Homa ya Mfuko wa Uzazi ni nini?
Ni magonjwa yanayompata mwanamke
katika uke, shingo ya uzazi,mfuko wa uzazi, mirija ya uzazi na sehemu
inayozunguka mfumo wa uzazi.
Karibu asilimia 85 ya watu
wanaopata homa hii hutokana na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana,
wengi wao wakiwa na vimelea vya bakteria kama vile kisonono (gonorrhoea),
kaswende (syphilis), klamidya n.k.
Wakati mwingine mgonjwa hupata
homa hii kutokana na bakteria ambao kawaida huwa wapo mwilini na hawana madhara
lakini kwa sababu mbalimbali kama kupungua kwa kinga, kisukari, saratani,
upasuaji, kuwa na magonjwa ya mfumo wa chakula n.k wanasababisha homa.
Dalili
- Maumivu makali chini ya kitovu na kiunoni,
- Maumivu wakati wa tendo la ndoa,
- Maumivu wakati wa kukojoa,
- Maumivu makali au kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi,
- Kutokwa na majimaji yenye harufu kali na rangi ya njano, kijani au kahawia ukeni,
- Kuwa na homa jotoridi 38.3 au zaidi,
- Kujisikia uchovu, kichefuchefu n.k.
Sababu
Homa ya mfumo wa uzazi mara
nyingi husababishwa na vimelea vya bakteria wanaambukizwa kwa njia ya tendo la
ndoa (sexually transmitted diseases -STD)
kama vile;
- Kisonono (Neisseria gonorrhoeae),
- Kaswende (Treponema pallidum),
- Klamidya (Chlamydia trachomatis ) n.k
Au kwa asilimia chache
husababishwa na vimelea wasioambukizwa kwa njia ya ngono.
Nani yupo hatarini kupata homa hii?
Kila mwanamke ambaye yupo kwenye
umri wa kuzaa anaweza kupata homa ya mfumo wa uzazi lakini kuna hali au vitendo
vinavyosababisha urahisi wa maambukizi kama vile;
- Kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja,
- Kufanya ngono zembe bila kutumia kinga,
- Kuwa na mpenzi mpya,
- Kama ulishawahi kupata homa hii au magonjwa ya aina hii kabla,
- Kushiriki ngono katika umri mdogo,
- Kama una umri wa chini ya miaka 25,
- Kama ulishawahi kufanyiwa upasuaji kwenye mfumo wa uzazi au mfumo wa mmeng’enyo wa chakula,
- Kama una vifaa vya kuzuia mimba kwenye mfuko wa uzazi ( intrauterin device ),
- Kutoa mimba kiholela bila kuzingatia hatua za kiafya au kupata mimba nje ya mfuko wa uzazi (ectopic pregnancy ),
- Kupata ajali n.k.
Wakati mwingine homa ya mfumo wa
uzazi inaweza kumpata mgonjwa siku, wiki, miezi au miaka mingi baada ya
kushiriki tendo la ndoa. Hivyo sio busara kuanza kushutumiana usaliti n.k
Uchunguzi
Ni muhimu sana ukipata dalili hizo hapo juu kwenda kwenye kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi. Kupuuzia kufanya hivyo vinaweza kumhatarishia maisha mgonjwa, kwani homa hii inaweza kuenea mwili mzima kwa njia ya mfumo wa damu ( sepsis).
Kuwahi kufanyiwa
uchunguzi pia kutampunguzia maumivu, kupata tiba kwa wakati na kutaepusha
madhara ya baadae kama ulemavu wa kudumu, utasa au hata kifo.
Mtaalamu wa afya atamuuliza mgonjwa vitu mbalimbali kama historia ya mapenzi, wapenzi, magonjwa mengine, umri n.k hivyo ni vyema kutoa taarifa zisizopotosha ili kuweza kupatiwa huduma zilizo sahihi.
Kwa wale wenye wapenzi ni muhimu kufanyiwa uchunguzi na
kupata matibabu ya pamoja ili kuondoa tatizo la kujirudia rudia.
Mtaalamu wa afya atamfanyia mgonjwa uchunguzi wa kina kama vile mkojo, damu, kupima mimba na kuchukua sampuli (swab).
Wakati mwingine vipimo vingine
kama ultrasound vinaweza kutumiwa ili kuangalia ukubwa wa tatizo na kuangalia
uwezekano wa kuwepo magonjwa mengine kama vile homa ya kidoletumbo (appendicitis), homa ya ukuta wa tumbo (peritonitis) n.k.
Tiba
Baada ya uchunguzi, daktari atamwanzishia mgonjwa dawa (antibiotics) zenye uwezo wa kuua bakteria zaidi ya mmoja au mchanganyiko wa antibiotics zaidi ya moja haraka iwezekanavyo wakati majibu ya sampuli yakisubiriwa.
Ni muhimu daktari kupewa taarifa kama mgonjwa ana wasiwasi wa mimba kwani kuna dawa zisizofaa kupewa mjamzito. Kawaida mgonjwa hupewa dawa hizi kwa muda wa wiki mbili, kisha kufanyiwa uchunguzi baada ya hapo ili kuamua kuendelea au kusitisha matibabu.
Wakati
huo huo mgonjwa atapewa dawa za maumivu na kushauriwa kula mlo kamili na kunywa
maji mengi. Wakati matibabu yakiendelea, haishauriwi kufanya tendo la ndoa.
Wakati mwingine mgonjwa anaweza
kulazwa hospitalini kwa uangalizi wa karibu na kupewa dawa kwa njia ya mishipa
ya damu (İ.V) kama yu mahututi, au
kama anashindwa kula na kunywa au endapo daktari atakuwa na wasiwasi wa huduma
ya mgonjwa akiwa nyumbani.
Nini kifanyike ili kuepuka homa
hii?
Kwa kuwa homa hii inaweza
kumsababishia mgonjwa madhara ( complications)
ya muda mrefu au ya kudumu kama vile; utasa,
homa kujirudia rudia, mimba za nje ya mfuko wa uzazi n.k, ni vyema
kujiepusha na tabia hatarishi kama ifuatavyo;
- Epuka ngono zembe,
- Epuka kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja,
- Epuka kufanya tendo la ndoa wakati wahedhi,
- Tumia kinga ili kuepuka maradhi,
- Jenga tabia ya kupima afya yako na mpenzi wako pale unapokuwa na dalili yoyote,
- Epuka kutumia dawa bila ushauri wa daktari,
- Epuka tabia hatarishi kama ulevi kupindukia, madawa ya kulevya yanayochochea vitendo vya ubakaji.
Maoni
Chapisha Maoni