Utangulizi
Kifua kikuu ni ugonjwa hatari sana unaosababishwa na vimelea vya bakteria vinavyoitwa Mycobacterium tuberculosis (MBT), wanaoshambulia sehemu mbalimbali za mwili hasa mapafu. Asilimia kubwa ya watu wenye kifua kikuu hawana dalili za kuugua (latent). Karibu asilimia 10 ya watu hawa hupata dalili baadae (active) na hatimaye nusu yake hufariki kwa ugonjwa huo.
Vimelea vya Kifua Kikuu huambukizwa kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa (kupumua).
Utafiti uliofanyika mwaka 2018 ulionyesha kuwa robo ya watu wote duniani wana vimelea vya Kifua Kikuu.
Mwaka 2020 watu karibu milioni 10 walipata Kifua Kikuu chenye dalili(active), watu milioni moja na nusu walifariki kwa Kifua Kikuu, kuufanya ugonjwa huu kuwa wa pili kwa kuua watu wengi duniani kwa magonjwa ya kuambukizwa ukiongozwa na COVID-19.
Nchi nane zinazoongoza kwa wangonjwa wa TBC ni India (27%), China (9%), Indonesia (8%), the Ufilipino (6%), Pakistan (6%), Nigeria (4%), na Bangladesh (4%).
Dalili
- Kikohozi cha wiki tatu na zaidi,
- Maumivu ya kifua,
- Kukohoa damu,
- Kuhisi uchovu muda wote,
- Kutokwa na jasho jingi usiku,
- Kupatwa na homa (jotoridi la mwili kupanda),
- Kupungua uzito,
Ukiwa na dalili kadhaa kati ya hizo hapo juu ni vyema kumuona daktari ili kupata vipimo na matibabu. Ikumbukwe kuwa Kifua Kikuu huambukizwa kutoka kwa mgonjwa pekee.
Una hatari ya kupata Kifua Kikuu kama;
- una rafiki au ndugu mwenye dalili,
- umesafiri nchi zenye wagonjwa wengi kama Urusi,Ulaya mashariki, Asia ya kati,Amerika ya kati, Afrika n.k
- Kama ni mhudumu wa afya, uko jela, ni mgonjwa wa UKIMWI, mtumiaji wa mihadarati au mvutaj wa sigara.
Una hatari ya kushindwa kupambana na active TBC kama;
- una UKIMWI
- una maradhi sugu kama vile Kisukari au ugonjwa wa figo,
- na saratani au unapata matibabu ya saratani,
- una utapia mlo .
Maambukizi
Kifua Kikuu huambukizwa kwa njia ya hewa kama vile mgonjwa ambaye tayari ana dalili(active) kukohoa, kuongea, kupiga chafya, kucheka, kuimba n.k. Hata hivyo maambukizi haya hayapatikani kirahisi, ni lazima uwe na ukaribu wa mgonjwa kwa muda mrefu. Huwezi kuambukizwa kwa kugusana, kupeana mikono, kula au kunywa pamoja au kwa tendo la ndoa.
Vipimo
Mtu menye dalili za Kifua Kikuu hufanyiwa moja ya vipimo vikuu viwili kutegemea na mazingira aliyepo.
- Kipimo cha ngozi: Muuguzi atakuchoma sindano ya majimaji yaitwayo PPD tuberculin mkononi na kuitwa baada ya siku 2 au 3 kuangalia uvimbe sehemu husika. Vipimo vikiwa chanya una uwezekano mkubwa wa kuwa na Kifua Kikuu japokuwa hauna dalili. Lakini pia kwa watu wenye chanjo ya Kifua Kikuu wanaweza kuwa na matokeo chanya danganyifu kutokana na chanjo hiyo.
- Kipimo cha damu: Muuguzi atachukua damu kwenda kuangalia kma damu yako inakingamana na TB protini.
Hata hivyo vipimo hivi havionyeshi kama wewe ni mgonjwa mwenye dalili (active) au asiye na dalili (latent). Kwa hiyo daktari atakufanyia kipimo cha picha ya kifua (chest x-ray) ili kujua kama mapafu yameathiriwa au la.
Kama utakuwa umeathiriwa na TBC daktari atakuanzishia dawa zaidi ya moja ambazo utalazimika kutumia kwa miezi 9 hadi 12 bila kupuuzia dozi.
Ili kupunguza maambukizi kwa watu wanaokuzungua kama ndugu,wahudumu au marafiki ni lazima kuzingatia maagizo ya daktari mpaka pale atakaposema upo kwenye hatua isiyoambukiza.
Hatua kadhaa zinaweza kuchukuliwa ili kupunguza maambukizi hasa mwanzoni mwa matibabu, kama vile;
- Kutumia dawa zote alizopewa mgonjwa kwa wakati,
- Kuhudhuria kliniki alizopangiwa na daktari,
- Kufunika mdomo wakati wa kukohoa, kupiga chafya, kuongea n.k, na kunawa mikono baada ya hapo,
- Kuacha kutumia usafiri wa umma,
- Kufungua madirisha ili kuongeza mzunguko wa hewa sehemu unayoishi,
- Epuka kutembelea watu au watu kukutembelea ukiwa kwenye kipindi cha maambukizi.
Katika nchi ambazo zina wagonjwa wengi wa Kifua Kikuu inashauriwa kupata chanjo ijulikanayo kama bacille Calmette-Guerin (BCG).
Maoni
Chapisha Maoni