Kukua Kwa Tezi Dume ( Benign Prostatic Hyperplasia) ni nini?
Ni ukuaji wa tezi dume ambalo lipo kwenye mfumo wa uzazi wa mwanaume hivyo kusababisha matatizo mengi hasa ya kibofu, figo na njia ya mkojo kwa ujumla. Hii hutokana na kuzibwa kwa njia ya mkojo kitu ambacho huleta madhara kwenye viungo husika. Tatizo hili huzidi kadri umri unavyoongezeka. Kwa kawaida ukubwa wa tezi ni sawa na kipira cha golf, lakini linaweza kukua hadi kufikia ukubwa wa chungwa hivyo kusababisha matatizo.
Tezi dume kazi yake ni kutoa majimaji ya shahawa (semen) yanayosaidia kulinda, kurutubisha na kusafirisha mbegu za kiume (sperms) ndani ya mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Karibu nusu ya wanaume wenye umri kati ya miaka 51 mpaka 60 na zaidi ya asilimia 90 ya wenye umri wa miaka 80 na zaidi wana tatizo hili. Ukuaji wa tezi dume sio saratani lakini wakati mwingine vyote viwili humpata mtu mmoja.
Dalili
- Kujisikia kukojoa muda wote au kushindwa kubana mjoko,
- Kukojoa kila mara hasa wakati wa usiku,
- Kuwa na shida wakati wa kuanza kukojoa,
- Kujisikia bado una mkojo hata baada ya kumaliza kukojoa.
Mara chache mgonjwa anaweza kukojoa damu, kupata maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo au hata kushindwa kukojoa kabisa. Wakati mwinginekuwepo kwa hizi dalili hakuendani na ukubwa wa tezi dume.
Kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi kama kuna matatizo mengine zaidi ya tezi dume kama vile; maambukizi ya njia ya mkojo, mirija ya mkojo kuwa myembamba, mawe kwenye kibofu au njia ya mkojo, saratani ya kibofu au tezi dume au makovu ya tezi kutokana na upasuaji au ajali.
Tezi dume lipo chini ya kibofu cha mkojo na huzunguka njia ya mkojo hivyo likikua linabana njia hiyo na kusababisha maumivu wakata wa kukojoa, kushindwa kukojoa kirahisi pamoja na dalili zote nilizoeleza hapo awali. Wakati mwingine mkonjwa hulazimika kwenda hospitali ili kuwekewa mrija maalumu wa kumsaidia kukojoa kwa muda
Watu wengi hasa wa umri wa miaka 50 na zaidi wana BPH lakini hawana dalili.
Sababu
Haijulikani kisayansi ni nini husababisha kukua kwa tezi dume, lakini wataalamu wanasadiki kuwa ni kutokana na homoni za kijinsia ndio hupelekea kukua kwa tezi dume.
Vitu au mambo yanayochangia kukua kwa tezi dume ni;
- Umri: Kadri umri unavyoongezeka ndio uwezekano wa kukua kwa tezi dume huongezeka,
- Nasaba: Inasemekana tezi dume huendana na vinasaba katika familia,
- Magonjwa sugu kama vile kisukari na magonjwa ya moyo huchangia kukua kwa tezi dume,
- Unene na unene kupindukia unachangia pia.
Mtu mwenye BPH ana hatari ya kuharibika kwa kibofu na figo ambavyo ni muhimu sana kwa mwili wa binadamu. Kuharibika kwa figo (acute renal failure), ni tatizo la dharura ambalo kama halitagunduliwa linaweza kumuua mgonjwa. Lakini kukua kwa tezi dume hakusababishi kupata saratani.
Uchunguzi
Pindi unapokuwa na dalili hizo hapo juu unashauriwa kufika kitua cha afya kwa uchunguzi. Daktari atakufanyia vipimo kadhaa ikiwemo mkojo ili kuondoa uwezekano wa kuwepo maambuki,
kuchunguza kwa vidole kupitia njia ya haja kubwa ili kutambua ukubwa, ugumu au ulaini wa tezi n.k.
Kipimo cha damu ili kuangalia afya ya figo.
Kulingana na umri daktari pia anaweza kuamua kupima kipimo kinachoitwa Prostate spesific antigen-PSA ambacho ni maalumu kwa ajili ya tezi dume
Vipimo vingine ni kama vile; Kupima mtiririko wa mkojo, ultrasound na sampuli (biopsy).
Tiba
Baada ya uchunguzi wa kina,daktari ataamua aina ya tiba atakayoanza nayo kulingana na mambo kadhaa kama vile, ubora wa afya yako, umri wako, ukubwa wa tezi dume, ukubwa wa dalili unazopata, kuwepo kwa saratani au la.
Kama dalili zinavumilika mara nyingi utashauriwa kuboresha afya yako kwanza kama vile kufanya mazoezi, kupunguza unene n.k babla ya hatua nyingine kama vile dawa au upasuaji. Utashauriwa kuhudhuria kliniki kwa ajili ya uchunguzi wa mara kwa mara.
Wakati mwingine daktari anaweza kumwanzishia mgonjwa dawa zinazosaidia kulegeza misuli inayozunguka njia ya mkojo. Hatua nyingine ni kama upasuaji wa kupanua njia ya mkojo, upasuaji wa kuondoa tezi dume au tiba kwa njia ya mionzi (lazer ablation) inayopunguza idadi ya chembehai za tezi dume.
Htua nyingine ni pamoja na kutibu maambukizi, kuondoa mawe ya kibofu au figo n.k.
Maoni
Chapisha Maoni