Utangulizi
Saratani ya Matiti ni nini?
Ni aina ya saratani inayoathiri matiti au maziwa kwa mwanamke au nadra pia kwa mwanaume. Hii hutokana na chembehai(
cells) za sehemu yoyote ya ziwa au yote mawili kukua kuliko kawaida na kusababisha uvimbe, maumivu, kutokwa na majimaji,damu au usaha kwenye matiti. Wakati mwingine aina hii ya saratani inaweza kusambaa sehemu nyingine za mwili kama vile kwenye kwapa, misuli ya kifua, mishipa ya damu, shingoni n.k.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2020, wanawake milioni 2.3 waligunduliwa kuwa na saratani ya matiti, takriban laki saba walifariki kwa saratani ya matiti. Kutoka mwaka 2015 hadi 2020 wanawake milioni 7.8 waligunduliwa kuwa na maradhi hayo, kuifanya saratani ya matiti kuwa ya kwanza kwa kuenea duniani.
Ni muhimu kutambua kwamba sio kila uvimbe uliopo kwenye maziwa ni saratani, hivyo ni vyema kumuona Daktari unapokuwa na dalili yoyote nitakayotaja hapo chini kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Nini husababisha saratani ya matiti?
Tofauti na saratani nyingine kama Ini, mlango wa uzazi n.k, saratani ya matiti si maradhi ya kuambukiza. Asilimia kubwa hutokana na kukua kuliko kawaida kwa chembehai (cells) zinazotoa maziwa, hivyo kusababisha uvimbe. Wakati mwingine chembehai hizi husambaa sehemu nyingine za mwili. Japokuwa sababu kamili haijulikani, wanasayansi wanaamini kuwa homoni, mtindo wa maisha, mazingira na vinasaba (genetics) zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata saratani ya matiti.
Tafiti zinaonyesha kuna vinasaba viwili breast cancer gene 1 (BRCA 1) na breast cancer gene 2 (BRCA 2) ambavyo ni vya kurithi na vinaongeza kwa kiasi kibubwa kupata saratani.
Nani yupo kwenye hatari ya kupata saratani ya matiti?
Kila mtu anaweza kuupata. Lakini kuna vitu kadhaa vinavyoongeza uwezekano wa kupata saratani ya matiti, kama ifuatavyo;
- Kuwa mwanamke,
- Umri: Kadri umri unavyoongezeka ndio uwezekano pia unaongezeka hasa miaka 40 na kuendelea,
- Kutokunyonyesha, kuchelewa kuzaa (miaka 30 au zaidi) au kutokuzaa,
- Kama uliwahi kuwa na saratani au uvimbe ambo sio saratani kabla,
- Kama kuna wazazi au ndugu wenye au waliwahi kuwa na saratani ya matiti,
- Mtumiaji wa pombe au sigara,
- Kupata hedhi umri mdogo (chini ya miaka 12) au kukoma hedhi umri mkubwa,
- Kuwa mnene au mnene kupindukia,
- Kuishi bila kufanya kazi za mikono au mazoezi.
Dalili
- Kuwa na uvimbe ambao upo tofauti na sehemu ya titi inayouzunguka,
- Kuwa na uvimbe kwenye kwapa, kifuani au shingoni,
- Kubadilika kwa ukubwa,umbo au mwonekano wa titi,
- Kubadilika kwa ngozi ya titi kama vile kuwa na rangi tofauti, mabaka mabaka au vidonda,
- Kubadlika umbo la chuchu kama vile kuingia ndani au kuwa ngumu yenye maumivu n.k.
Ni kawaida kwa wasichana wadogo kuwa na uvimbe wa muda kwenye matiti kama vile wakati wa hedhi.
Nini kifanyike ili kujikinga?
Kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha ya kila siku itasaidia sana kuepukana saratani ya matiti.
Mambo yafuatayo yanafaa kuzinatiwa;
- Kufanyiwa vipimo vya mara kwa mara pamoja na kupewa elimu ili kuweza kujifanyia uchunguzi mwenyewe,
- Kufanya mazoezi angalau nusu saa kila siku,
- Kula mlo kamili kunywa maji mengi ambayo ni safi na salama,
- Kuepuka kunywa pombe na kuvuta sigara,
- Japokuwa ni changamoto kwenye jamii tuliopo, kutambua kuwa mionzi ya simu inasemekana kuwa na athari zake,
- Kuhakikisha unajiendeleza vizuri kiafya na kuepuka unene na unene kupindukia.
Tiba
Sehemu hii ni ya kitabibu zaidi hivyo ni vigumu kuielezea hapa lakini kwa muhutasari tu ni kwamba, tiba ya saratani huanzia kwenye hatua za kujikinga nilizozitaja hapo juu.
Pamoja na hayo daktari atakufanyia mlolongo wa uchunguzi na vipimo mbalimbali kama vile uchunguzi wa mikono mara kwa mara, vipimo vya ultrasound na mammogram.
Pale ambapo atahisi kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina zaidi wakati mwingine atakuchukua sampuli kwa sindano maalumu (biopsy) ili kutambua aina ya chembehai ambazo zitasaidia kuamua hatua na aina ya tiba.
Vipimo vingine kama damu, CT- scan, MRI, PET-scan n.k pia vinaweza kufanywa.
Hatua zinazofuata ni pamoja na upasuaji ili kuondoa uvimbe na pamoja na tishu zinazozunguka, tiba ya dawa (chemotherapy), mionzi (radiotherapy) n.k, kulingana na aina ya saratani pamoja na hatua iliyopo wakati wa uchunguzi.
Kwa mgonjwa wa saratani ya matiti
Pamoja na kwamba saratani ni maradhi yanayotisha mioyo ya watu ni muhimu kutambua kwamba saratani ya matiti inatibika kwa asilimia kubwa. Uchunguzi wa mapema ni jambo la muhimu sana. Ni muhimu kushirikiana na wataalamu afya. Mambo mengine ni pamoja na kuepuka msongo wa mawazo, kufanya mazoezi, kuhudhuria kliniki katika hatua zote.
Kwa ndugu jamaa na marafiki, kumpa msaada wa hali na mali mgonjwa sio tu kutampandisha morali lakini pia kutamsaidia mgonjwa kupona.
Maoni
Chapisha Maoni