Ualbino ni nini?
Ualbino (albinism) ni hali ya kiafya inayotokana na mwili kukosa uwezo wa kutoa homoni aina ya melanin. Homoni hii pamoja na kazi nyingine inahusika na utoaji wa rangi ya mwili. Ukosefu wa melanin huathiri ngozi, macho na nywele.
Ualbino ni hali ya kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ikumbukwe kuwa Albino sio mgonjwa bali ni mlemavu wa macho, nywele na ngozi ambavyo huathiri maisha yake ya kila siku, hata kufupisha umri wa kuishi. Nje na binadamu ualbino unaathiri pia wanyama, samaki, wadudu, nyoka, mijusi, ndege na hata mimea (kwa mimea hutokana na ukosefu wa klorofili).
Waathiriwa wenyewe nchini Tanzania waliamua kupendelea kuitwa "watu wenye ualbino" kutokana na matumizi mabaya ya neno zeruzeru katika utamaduni wa Afrika ya Mashariki ambako watu mara nyingi waliona uhusiano kati ya waathiriwa na mapepo au mizimu.
Kuenea kwa Ualbino
Tafiti zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya 20,000 duniani ni albino, lakini kwa sababu zisizofahamika barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara kuna idadi kubwa zaidi ya albino kuliko kokote duniani. Kwa mfano inasadikiwa kwa nchini Tanzania kuna albino mmoja kwa kila watu 1,400. Nchi ya Zimbabwe inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi, ikiwa na albino mmoja kwa kila watu 1,000.
Asili
Albino huzaliwa na hali ya kukosa uwezo wa kujenga homoni ya melanin ambayo ni muhimu kama kinga dhidi ya mionzi ya jua. Watu wenye ualbino huwa na nywele nyeupe au njano, na ngozi nyeupe. Macho yao ni bluu au hata pinki.
Uwezo wa kutengeneza homoni au pigimenti ya melanin hutegemea vinasaba (genes) vya kurithi. Vinasaba hivi vikiwa vibovu ndio husababisha mwili kushindwa kutoa melanin.
Ikumbukwe kuwa vinasaba hivi vibovu hubebwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kwa kuwa vinasaba hivi vinatoka kwa baba na mama, inamaanisha kwamba mtu huzaliwa albino kama wazazi wote wawili tayari wana vinasaba vibovu. Wazazi hao wote wanaweza kuwa ni wabebaji tu na sio albino. Watoto wengine pia wanaweza kuwa sio albino. Hali hii inaendelea katika familia na inaweza kuonekana mara kwa mara inategemea na kupatikana kwa vinasaba husika katika wazazi wote wawili.
Dalili
Ni rahisi kumtambua albino kutokana na ngozi na nywele zake kuwa nyeupe kuliko kawaida.
- Kupata majeraha kirahisi na pia kuchelewa kupona,
- Kupata majeraha baada ya kukaa muda mrefu juani,
- Kuwa ma mabaka meusi ambayo hutokwa na damu kirahisi,
- Nywele nyeupe, nyekundu au kahawia,
- Macho ya bluu au pinki.
Kutokana na macho kushindwa kuchuja mwanga wa jua kwa kukosekana au upungufu wa melanin kwenye mboni, hali hii huathiri sana uwezo wake wa kuona. Vilevile hushindwa kutambua ukaribu au umbali wa kitu na kutofautisha rangi. Hii inaweza kuwa hatari hasa kwa magari na taa za barabarani.
Tiba
Kwa bahati mbaya ualbino ni hali isiyotibika. Tiba yake hulenga zaidi kwenye vitu au hatua zinazochukuliwa ili kuboresha maisha yake kama vile kuona na kinga dhidi ya jua au majeraha.
Mambo kadha kama yafuatayo yanaweza kufanywa;
- kufanyiwa vipimo vya macho mara kwa mara na kupatiwa miwani maalumu inayorekebisha kuona na kupunguza mwanga.
- kufanyiwa vipimo vya ngozi kila mwaka ili kutibu majeraha pamoja na kugundua endapo kuna madoa yanayoweza kuwa na tabia ya saratani ya ngozi kutokana na mionzi mikali ya jua.
Albino anaweza kufanya yafuatayo ili kujilinda yeye mwenyewe;
- Kuvaa miwani ya jua (sunglasses),
- Kuvaa nguo zinazoakisi mwanga na kumlinda kutokana na mionzi,
- Kupaka mafuta malumu yaliyotengenezwa kwa ajili ya kupunguza athari za mionzi ya jua,
- Kuepuka tabia hatarishi kama vile ulevi, mihadarati, ugomvi n.k,
- Kupunguza kutoka nje wakati wa jua kali au kutumia kofia pana au mwamvuli.
Kwa wanafunzi hasa wa shule za msingi, ni muhimu walimu kuwaelimisha wanafunzi wenzake juu ya hali ya albino ili kushirikiana nae katika kuboresha maisha yake.
Hatua zingine ni kama vile;
- kuepuka unyanyapaa,
- kukaa dawati la mbele,
- mwalimu kuandika kwa maandishi makubwa,
- kutumia daftari lenye rangi iliyofubaa ili kupungua kuakisi mwanga, pia kuepuka kutumia rangi mbalimbali katika maandishi,
- kuweka mapazia darasani na kupunguza mwanga( taa za umeme za kwenye dari),
- kumpa muda zaidi hasa wakati wa mtihani.
Hitimisho
Kwa bahati mbaya katika jamii nyingi hasa katika bara la Afrika kumekuwa na imani duni za kishenzi zinazohusisha ualbino na mapepo, mizimu au ushirikina. Hapa kwetu Tanzania, Burundi n.k kumekuwa na imani potofu kuwa viungo vya albino vinaleta bahati kama vile mali, hivyo kusababisha mauaji ya kikatili yasiyokubalika ya albino. Ni changamoto ya kila binadamu kutoa elimu sahihi juu ya suala hili ili kulinda maisha wa wenzetu wasio na hatia.
Asante sana kwa makala nzuri Daktari bila shaka tunaruhusiwa kushare na wengine keep it up
JibuFuta