Fistula ni nini?
Fistula ni tundu lisilo la kawaida ambalo hutokana na kuungana kwa sehemu ya chini ya utumbo mpana (njia ya haja kubwa) na njia ya mkojo au njia ya uke, hivyo kumfanya mgonjwa kushindwa kuzuia haja au kutokwa na hajakubwa ukeni. Mara nyingi husababishwa na kujeruhiwa kwa sehemu hizo wakati wa kujifungua hasa kwa wanawake wanaozaa katika umri mdogo au wanaokosa msaada stahiki wakati wa kuzaa.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na Asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote, kwa upande wa Tanzania wengi wamekua wakitafuta msaada kwa waganga wa jadi.
Nini Husababisha Fistula?
Ugonjwa wa Fistula unaweza kusababishwa na mambo kadhaa ikiwemo yafuatayo;
- Majeraha wakati wa kujifungua,
- Maambukizi ya Mfumo wa uzazi (PID),
- Mgonjwa ya utumbo mpana kama vile Crohn ,
- Saratani ya mfumo wa uzazi au utumbo mpana,
- Majeraha yanayotokana na ajali au upasuaji wa sehemu ya nyonga.
Fistula husababisha mwanamke kukosa furaha, kupata maambukizi ya mara kwa mara ukeni,kukosa kujiamini na kukata tamaa hasa katika ndoa.
Dalili za Fistula
- Kutokwa na haja kubwa ukeni,
- Kuwa na harufu mbaya muda mwingi ukeni,
- Kupatwa na maambukizi ya mara kwa mara ukeni,
- Kujisikia maumivu ya nyonga mara kwa mara, hasa wakati wa tendo la ndoa.
Uchunguzi
Pindi unapokuwa na dalili hizo hapo juu unashariwa kumwona daktari kwa uchunguzi zaidi.
Tegemea daktari kukuuliza maswali ya kina kama vile dalili ulizonazo, lini zimeanza, je dalili hizi zipo muda wote au hutekea mara kwa mara, kama zilianza baada ya kuzaa au la, kama zinapungua au kuzidi, kama ulishawahi kufanyiwa upasuaji kabla au la?
Daktari atakufanyia uchunguzi kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuangalia kama kuna uvimbe, kidonda au dalili yoyote ya saratani. Vingine ni kama vile kuangalia kwa vifaa maalumu ili kuona kama kuna tundu la fistula kwenye kibofu cha mkojo au kwenye ukuta wa nyuma wa uke. Kingine ni kwamba daktari anaweza kuingiza maji ya rangi kwenye njia ya haja kubwa na kuweka tampon ukeni na baadae kuangalia kama rangi hiyo imeenda mbele au la.
Hatua nyingine zinahusisha kufanyiwa vipimo vya mionzi (X-ray) kwa baada ya kuingizwa kwa kemikali maalumu zinaoonekana kwenye X-ray yaani contrast zitakazosaidia kuona kama kuna tundu.
Vipimo vingine ni kama CT-scan, MRI n.k.
Tiba
Baada ya daktari kujiridhisha na vipimo kuwa mgonjwa ana fistula,mara nyingi njia pekee ya kupambana na tatizo hili ni upasuaji ili kuziba tundu. Hivyo kwa asilimia kubwa mgonjwa atashauriwa kufanyiwa upasuaji.
Kabla ya upasuaji endapo mgonjwa ana maambukizi katika kipindi cha uchunguzi basi atapewa dawa (antibiotics) kwanza ili kupambana na maambukizi kisha kupanga upasuaji kulingana na hali yake ya kiafya.
Maswali ya msingi ambayo mgonjwa anafaa kumuuliza daktari wakati wa uchunguzi ni kama vile:
Nini kimesababisha fistula, nini kinasababisha dalili alizonazo, je ni tatizo la muda au la kudumu, nini kifanyike ili kuondokana na tatizo hili au kupunguza dalili za tatizo hili? Vitu vingine ni kama vile Namna gani ya kutibu fistula au dalili hizi endapo upasuaji hauwezekani kutokana na sababu mbalimbali?
Je, mgonjwa afanye nini akiwa nyumbani?
Kwa mgonjwa ambaye tayari amebainika na fistula na anasubiri tiba anatakiwa azingatia mambo yafuatayo akiwa nyumbani;
- Kuosha sehemu za nje za siri kila mara anapohisi kutokwa na maji maji,
- Kuepuka kutumia sabuni ndani ya uke wakati wa kuosha,
- Kila anapoosha ahakikishe anakausha kwa kitambaa kisafi,
- Aepuke kuvaa nguo za ndani zinazobana na anashauriwa kutumia chpi za pamba ili kuruhusu mzunguko wa hewa,
- Kama tatizo ni kubwa anashauriwa kutumia pedi na kuzibadilisha mara kwa mara
Jamii kwa ujumla inafaa itambue ukubwa wa tatizo hili na kuwapa msaada wa hali na mali wagonjwa. Mtu wa kwanza kumpa msaada mgonjwa ni mume wake, mzazi wake na ndugu zake wengine.
Hivyo familia nzima inafaa kushirikishwa kwenye hatua zote za matibabu ili kumpa moyo mgonjwa na kuondoa unyanyapaa. Hili sio tatizo linaloweza kutibiwa kwa waganga wa kienyeji kwani linahitaji upasuaji.
Maoni
Chapisha Maoni